October 23, 2018

Wafungwa Wasile Chakula cha Bwerere: Nkaissery

Kenyan-inmates-sing-and-dance-during-an-inter-prison-competition-held-at-Naivasha-Kenyas-biggest

Imetafsiriwa na; FLORENCE CHANYA

Waziri wa usalama na mambo ya ndani, Bwana Joseph Nkaissery amesema ya kwamba hakitakuwepo chakula cha bwerere kwa wafungwa wanapotumikia vifungo vyao. Alisisitiza kuwa itakuwa bora kama watatengeneza barabara ili kupunguza gharama ya kuyakimu mahitaji yao.

Waziri alisema kuwa wanapaswa kuhusishwa katika miradi ya maendeleo ambayo kwa sasa inafanywa na vibarua walioajiriwa na wasimamizi wa miradi hiyo. “Nitatoa mapendekezo ndiposa wafungwa wakome kula mlo wa bwerere gerezani. Watakuwa wakitengeneza barabara,” aliongeza.

Halikadhalika ni maoni yake pia, kuwa wafungwa watengewe pesa na serikali pindi wapatapo uhuru ili ziwafae katika kuufungua ukurasa mpya wa maisha yao. Vile vile aliwahimiza wafungwa kuyatilia maanani mafunzo wanayopata wanapotumikia vifungo kwani watayahitaji watokapo gerezani.

Nkaissery alikuwa akizungumza haya katika ziara yake ya kwanza kabisa ya magereza humu nchini. Alianzia na gereza la Malindi, katika kaunti ya Malindi. Mbunge wa huko, Bwana Dan Kazungu, na kamishna wa magereza wa sehemu hiyo, Bwana Samuel Kilele, pamoja na maafisa wakuu wa usalama waliandamana naye.

Kuimarishwa kwa Vituo

Nkaissery aliahidi kupanga mikakati ya kuimarisha hali ya magereza. Alisema haya alipoiona hali ya seli. Hata hivyo aliwaonya wafungwa dhidi ya kuurejelea uhalifu uliowasababishia kutiwa mbaroni; akisisitiza kuwa, kuna njia nzuri za kuihudumia jamii.

Mbunge wa Malindi, Bwana Dan Kazungu alisema kwamba, hivi karibuni wafungwa watasaidia kuunadhifisha mji ili utalii unoge. Naye waziri akatoa ahadi ya kuendelea kuyazuru magereza ili kuhakikisha kuwa yapo katika hali nzuri. Zaidi ya hayo alidokeza kuwa serikali ina kila nia ya kuibadilisha hali ya magereza ili iwafae wafungwa.

Related posts