October 23, 2018

UPEO WA MACHO UNGALI UNAITA

old woman

Imetafsiriwa na; FLORENCE CHANYA

Upeo wa macho bado unaita. Sauti imepazwa kuliko awali. Hamu ya kumsaka babangu inaongezeka kwa vishindo visivyomithilika. Nimetuwama pale pale nilipokuwa miaka mingi iliyopita. Dirisha lingali linaangaza miale ya upeo wa macho. Virago vyangu nimevifunga. Naja babangu. Nitakachokikuta huko sikijui, ila ninapiga hatua ya imani. Mamangu mwenyewe hana chochote ila picha yako tu.

Uso wako mtanashati na tabasamu ndivyo ninavyoandamana navyo unyo unyo. Nikijiuliza sababu yako ya kutuacha. Tumelandana sana. Je maisha yamekunyanyasa au ungali mtanashati? Je, una tumbo kama kiriba au u buheri wa afya? Je wewe ni sawa na mwanamume mtanashati ninayemwona pichani na mtindo wa nywele uitwao ‘Mohawk’? Naam, kabla ya kuyajua hayo na mengine, nitakapokuwa safarini, ningependa uyafahamu mambo machache tu yanayohusu maisha yangu.

Mama aliniambia ya kwamba ulitutelekeza. Niliishi tu, bila chochote cha kuwaambia marafiki wangu kuhusu baba mzazi. Ilibidi nijitie moyo kwani sikuwa na njia ya kukurejesha. Siku yangu ya kwanza shuleni niliogopa kuulizwa shughuli yako ya maisha. Kwa hivyo nililikwepa darasa kwa wiki moja kwa kujifanya mgonjwa. Mama alinipeleka kwa madaktari. Ugonjwa wakaukosa. Wazee wa kanisa wakakusanyika waniombee. Waumini wakayapigania maisha yangu kiroho. Wakaniwekelea mikono wakinitakia uzima na kukipiga kifo pute. Lakini, baba nilikufa kitambo. Fikira za kutokuwepo kwako kuliiondoa maana ya maisha.

Baba, natumai utajivunia mwanao kwani nilikuwa mwerevu tokea nilipokuwa wa umri mdogo. Ningependa kuhusisha hilo na wewe; kana kwamba akili hurithiwa. Yote hayo ni kwa mujibu wa babake mwandani wangu ambaye ni DDO(Daily Drinking Officer) kumaaanisha afisa anayepiga mtindi kila uchao. Kila kukicha afisa huyu humlaumu rafiki yangu kwa kuurithi upande wa mamake na ndiposa akawa mjinga. Nashindwa kuelewa kama madaktari ni wajinga kwani mamake sahibu yangu huyu ni daktari. Ukweli usemwe babangu, bora rafiki yangu abaki mjinga machoni pa abuye, kuliko kuurithi upande wa babake, kwani atahitimu na shahada ya uzumbukuku.

Kama nilivyokuwa nikisema, nilikuwa mwerevu na nilifahamu fika kuwa baada ya kuombewa hivyo; vitendo vya waumini hao kutompumzisha Rabuka, wakiniombea mimi, vingejibu, kwa hivyo wiki ya pili niliamka mwenyewe na kwenda jikoni kumwamkua mama. Alibubujikwa na machozi, akayashuhudia matendo ya Mungu na kumwita Mhubiri ambapo kwa mara ya pili alimkubali Kristo kwa miujiza aliyotendewa na Maulana. Angalao ninamfahamu mmoja atakayenifuata mimi kwenye foleni ya hukumu. Naskia matendo yetu yatatufuata.

Basi nikaenda shuleni, nikavuta pumzi. Mama akanishika mkono, tukitembea sako kwa bako. Laiti ungekuwa wewe,baba. Laiti umgemwona Kinjunya alivyotembea kwa majisifu kando ya babake. Akifahamu kuwa babake alikuwa mlinzi wake. Misuli ya abuye hiyo haikuwa bure bilashi. Lakini upande wangu mamangu alinieleka kama mtoto. Akanidekeza. Kujisifu kwangu kungetokana tu na msumari uliopakwa rangi ya kucha na mwanasesere aliyeniachia mama.

Ama kwa kweli baba, huo ni uungwana? Mtu atamlea vipi simba kama kuku wa kizungu? Jambo hili linaitesa hulka na mwelekeo wa maisha. Katu siwezi kumlaumu mama. Ni tatizo la ulezi, kwa hivyo ninaelewa. Wazazi hudhania kuwa, kwa kuwadekeza watoto wao watayasuluhisha mengi. Wanadhania kuwa hii ndiyo njia pekee ya kulea. Wengi husita kuwaadhibu watoto wao, wakisema watatumia njia mbadala. Ati watawafungia chumbani. Kumfungia mwanao chumbani ni sawa kumwambia akalale.

Laiti mamangu angeufahamu ujanja huu, singejifanya mgonjwa awali na hawagemsumbua Rabuka. Ningeenda shuleni wiki ya kwanza kama wengine; lakini kwa kuwa nilidekezwa, hujiuliza ungekuwapo ungefanyaje. Je, ningeenda shuleni siku hiyo ya kwanza? Je, ningebembea kwenye misuli yako na kuichezea suruali yako ya jinzi?

Baba, ulinipoka siku yangu ya kwanza, na ndio kwanza mkoko unaalika maua.

(Tafsiri ya Horizon: A Stolen Boyhood 2 iliyoandikwa na Mwangi Macharia)

Related posts