October 23, 2018

UONGOZI: CHANGAMOTO YA KUWA ZAIDI YA WASTANI

mandela leader

Imetafsiriwa na FLORENCE CHANYA

Mwenye subira, mwaminifu, anayeweza kushirikiana na wengine. Hizi ni sifa chache tu, kutoka kwenye orodha ndefu ya sifa zinazofaa kumilikiwa na kiongozi halisi. Uongozi ni wa njia nyingi, kutoka kwa kiongozi wa jamii hadi kwa rais. Nafasi hizo zote za uongozi zinahitaji kiwango kikubwa cha maadili mema ili kutekeleza majukumu ndiposa malengo ya viti hivyo vya uongozi yafikiwe. Kwa kipindi, mtindo umetokea ambapo viongozi washabikiwao wamechipuka kutoka miaka ya kisogoni ya kung’ang’ania uhuru, watu walipokuwa wakijaribu kuitambua nafasi yao kama katika uhuru na mabadiliko.Tunawaamini wanawake na wanaume hawa kwa minajili, mara si kidogo; wameonyesha nia ya kuiweka nchi mbele ya nafsi na mahitaji yao. Wanathaminiwa na kila mtu. Nelson Mandela hakuwa rais mweusi bali baba wa taifa. Mahatma Gandhi hakuwa mhindi mtetezi wa haki za Mwafrika-Mmarekani kwa kuwa alizitetea haki za binadamu dunia nzima. Hawa na wengine; walikuwa viongozi kindakindaki.

Viongozi hawa walishabikia umoja na vitendo vyao vilikusudiwa kuhamasisha umoja miongoni mwa wafuasi wao. Hata hivyo uongozi huo umezikwa katika kaburi la sahau. Hii inamaanisha ya kwamba hatuna viongozi tunaoweza kufuata nyayo zao leo hii, au ni swala la kutafuta sifa zinazofaa kwa wasiofaa?

Leo uongozi unaonekana kutumbukia nyongo. Zilikuwepo, lakini zimepita siku za viongozi kuwa watu ambao jamii ingeweza kufuata nyayo zao. Viongozi ambao waliweka viwango vya juu vya mahusiano kati yetu sisi. Ukwasi, nafasi na kujulikana kama pesa ndiyo njia mpya ya kuwatambua viongozi kabla ya kuwapatia wadhifa. Hakika kama vilivyo vidole vya mkono wa mtu wa kawaida, hatutoshani na hivyo viongozi watarajiwa hutumia njia mbadala kuzimiliki sifa hizo nilizotaja. Njia hii ya kuwapaka rangi ile wakubalike inaonekana kufanya uharibifu kuliko wema kwani watu wanayapoteza maisha yao huku hulka zikipata sifa mbaya, kinyume sana na matarajio. Chukua kwa mfano, kampeni za kiongozi wa wanagenzi wa chuo kikuu. Mfano mzuri unaokaririwa sana ni wa uchaguzi moto na kampeni za chuo kikuu cha Nairobi.

Kinyang’anyiro chao huwa moto wa kuotea mbali zaidi kikilinganishwa na cha uchaguzi wa kitaifa wenyewe. Uongozi, hasa katika siasa umebadilishwa ukawa uga wa mchezo wa “nani anamjua nani.” Kuundwa kwa miungano badala ya kuuzwa kwa sera kumekuwa jambo la kawaida nyadhifa zinapowaniwa.Kama ilivyo sasa katika chuo kikuu cha Nairobi, kusuhubiana na kiongozi wa sasa wa wanafunzi, Paul Ongili Owino; ama kwa lakabu Babu Owino; kunakuwa hakikisho la wadhifa huo mkuu unaomezea mate. Jambo hili linaonekana papai kwa kijiko lakini hebu subiri…kuna kizingiti. Kabla ya kukimbia hapa na pale, ukijaza matumaini, lazima uyafahamu mambo yanayoandamana na nafasi kama hiyo ya uongozi.

Ikiwa unahitaji ukweli mtupu, vyombo vya habari vinatosha. Vitakufanyia kazi murua kwani hivi karibuni vimeliangazia jambo hili. Ukitaka kukutana ana kwa ana na kifo, wania wadhifa kama huo wa kiongozi katika vyuo vikuu vya kutajika huku Kenya, hii leo.Bwana Dennis Njeru alikata shauri kuuwania wadhifa wa Babu ambaye ameukwamilia kutoka mwaka wa mbili elfu na kumi na moja.Picha zake, akivuliwa nguo katika mitaa ya Nairobi hazikusita kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.Na vitisho vya kutolewa uhai ndivyo vinavyomkabili mkabala katika azma yake ya kuwania uongozi.Jambo hili linaweza kukuduwaza duduvule kwa kuwa limeripotiwa kutoka katika chuo kikuu, lakini katika mchezo wa kawaida wa siasa katu sio la kuajabia. Ndiposa tunasaili, mbona mtu akipoteze kichwa chake kwa ajili ya wadhifa fulani? Kwa nini mtu apige masafa marefu namna hiyo akiishia kuwa juu kidogo tu, ya wastani? Kuna haja gani?

Kiongozi halisi hunyenyekea kiasi cha kukubali makosa yake. Lakini pamwe na kiburi kilichowagubika wanasiasa wa Kenya ni “ kiongozi” yupi atakuwa mwoga wa kutosha kuomba msamaha kwa makosa yaliyofanywa?Kwa maoni yangu, tukio lenye utata la Charles Keter huko Gilgil; kwenye daraja, ni mfano mwafaka wa matumizi mabaya ya uongozi. Wakenya wenye fikira kama zangu bado wanamsubiri “mheshimiwa” awatake radhi, sawa na waumini wanavyosubiri kuja kwa Masihi aliyeahidiwa. Mbona mambo haya hayafanyiki katika Kenya ya Leo?Kwa nini tutoe rushwa ili tupate nafasi? Kwa hakika wanasiasa wa Kenya wamefanya gange bora katika kuwapotosha viongozi wa kesho. Si wakati umefika wa kujifunga kibwebwe, tukate shauri kuwa- hatutaki tena?

Jack Welch alisema kuwa, kabla ya kuwa kiongozi ushindi unapatikana katika kujijenga mwenyewe, na unapokuwa kiongozi ushindi upo katika kuwajenga wengine. Viongozi wa siku za usoni wakome kutafuta mali uongozini. Na wasipende kuongoza kwa kuwa wameshawishiwa tu. Viongozi halisi huleta mabadiliko na wala si kufuata mifano hafifu iliyoachwa na waliowatangulia. Katika kuchagua viongozi wa nyanja zozote zile, tukumbuke kuwa hulka na maadili mema ya kiongozi ni muhimu, la sivyo tutaishia kuwa na matukio ghasi anapokuwa ofisini.

Mwisho nawasihi viongozi wote watarijwa wahakikishe kuwa wanawajibika na kukoma kutoa vijisababu, wanapochukua hatamu za uongozi. Kila mtu hawezi kuwa kiongozi. Uongozi hauwezi kupeanwa, lazima mtu astahili kuupata. Mja hawezi kupokwa uongozi , bali huupoteza kwa kutofanya kazi nzuri kama inavyostahili.

Tafsiri ya: Leadership: the challenge to be something more than average
Ya, Jeanne Ongiyo

Related posts