August 19, 2018

TAIFA LA WALAJI KUKU

Wadau wakuu kwenye sakata ya kuku wamezua mijadala mikubwa miongoni mwa wakenya. Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi na Mipaka Iscaac Hassan, waziri wa kawi Davis Chirchir,aliyekuwa mkurugenzi mkuu waIEBC James Oswago na bwana Paul Wasanga wamehusishwa pakubwa na sakata hiyo iliyomshirikisha Trevy Oyombra kwa madai ya kupokea rushwa ya milioni kati ya mwaka wa 2008 na 2010 pamwe na zabuni ya kuchapisha karatasi za mitihani ya kitaifa.
Madai ambayo bwana Hassan, Chirchir na Wasanga wamekana walipofika kwa tume kupambana na ufisadi na maadili EACC, Hassan alivilaumu vyombo vya habari kwa kueneza dhana ya kuwa aliwajibika pakubwa kwa sakata hiyo. Vile vile bwana Chirchir alisema yuko tayari kujiuzulu endapo atapatikana na hatia lakini kama wasemavyo waswahili mwizi huwa hajidumbi.

Natilia shaka endapo tume ya EACC chini ya mwenyekiti wao Mumo Matemu, wataweza kukabiliana na zimwi hili la udfisadi. Duru za kuaminika zinasema bwana Matemu alidai kuwa hawatatumia ushahidi uliowafunga washukiwa wakuu wa sakata hiyo huko uingereza na ile ya kampuni ya Ouzman na badala yake wataanzisha uchunguzi wao ili kubaini mbivu na mbichi.
Nahisi wakenya wanachezewa shere kwenye sakata nzima je tume ya EACCinahitaji nini zaidi ili kuwatia mikononi jamaa hawa? Chambilecho mbunge wa Nandi Hills Alfred Keter  “are they waiting a call for Jesus Christ or god?” naye bwana Adan Duale kiongozi wa walio wengI bungeni angewaambia “hii kuku si ya mama yenu bwana”
Ufisadi kwa miaka na mikaka umezagaza mizizi ambayo wadau wengi wameshindwa kuikata kila uchao tunaskia visa vya ufisadi ila hatuoni yeyote akitiwa mbaroni aende kula maharagwe chambilecho Raila Odinga.
Itakumbukwa juzi katibu mkuu wa chama cha ODM na mbunge wa Budalangi Ababu Namwamba aliponea tundu la sindano baada ya wenzake kushindwa kumtimua kwa madai sawia na hayo,kikawa sasa kisa cha kuona kibanzi machoni mwa mwenzio ukasau boriti ulionayo machoni.

Inadaiwa kuwa Namwamba alizicheza kanda zilizokuwa zimewarekodi wenzake kwa kupokea mlungula hivyo wakaghairi na kubatilisha msimamo waliokuwa nao hapo mwanzoni.
Hata kabla umande haujakauka au kuku kumeza punje sakata ya Mumias inayowahusisha wadau wakuu kwenye serikali ya kaunti ya Nairobi imekuwa kiazi moto na jambo la kuatua moyo.

Mabilioni ya pesa zilizoingia mifukoni mwa matapeli na wafisadi hadi sasa haijanbainika ni nani mla kuku?
Nakumbuka serikali ya Jubilee iliposhika hatamu za uongozi iliwaahidi wakenya kuwa itashughulikia masala na masaibu wanayokumbana na nayo lakini mambo yameenda kinyume na ahadi hizo za kampeni.

Ufisadi umeingia pote si upinzani si serikali.  Je ni nani wa kuaminika kenya hii?
Hayawi hayawi huwa ila tume ya EACC imechelea sana kuwatia mikononi wafisadi hayo ni tisa kumi je uchunguzi wa mauaji ya mbuge wa kabete George Muchai umeisha?

Nna je kiini na chanzo cha kifo aliyekuwa seneta wa Homabay marehemu Otieno Kajwang na marehemu Mutula Kilonzo je? Tunaandikia mate na wino ungali upo? Tunalaumu wakwezi na mnazi umeliwa na mwezi…tafakari hayo…

Related posts