October 23, 2018

Songombingo la mfumo wa kidijitali

Fred_Matiangi_5

Mvutano baina ya wadau husika kwenye sekta ya mawasiliano umeendelea kutokota kwa muda huku kiazi moto kikiwa mfumo wa kidijitali ambao umendelea kuzonga vyombo vinne vya habari. Haya yanajiri siku chache baada mahakama ya juu kutoa uamuzi wake ambapo mamlaka ya mawasiliano nchini CAK ilitoa taarifa kwamba runinga zote ambazo hazikuhamia mfumo wa kutangaza wa dijitali zingezimwa jambo ambalo lilipelekea kampuni zote kupokonywa masafa ya analogi.

Lakini je mvutano huu utaendelea hadi lini? Hapo jana waziri wa mawasiliano na teknolojia  bwana Fred Matiangi  akiwa mbele ya kamati ya bunge, ambapo alijikusuru kujiondolea lawama  kuhusiana mzozo ambao umezidi kupanua nyufa, alieleza hisia zake kwa kina. Bwana matiangi aliapa kuwa hawatalegeza msimamo wao japo alisisitiza kuwa walikuwa tayari kuketi na wadau walioathiriwa ili kutafuta muafaka kuhusiana na mfumo wa kidijitali.

Vile vile mamlaka ya CAK imetoa onyo kuwa vyombo hivi vya habari vilikwenda kinyume na makubaliano ya korti kwa hiyo wameandaa mikakati  ya kuwasilisha kesi mahakamani  ili kuvishtaki vyombo hivyo.  Zogo hili lilijiri  wakati ambapo wakuu wa stehseni za runinga mbili nchini waliagizwa kufika mbele yao kwa kukiuka maagizo na kurejea katika mfumo wa analogi.

Itakumbukwa kuwa katika uamuzi  wa mahakama kuhusiana na mchakato mzima  wa kidijitali , majaji wa mahakama ya juu waliamrisha mamlaka ya mawasiliano nchini kurejesha leseni za digitali kwa runinga kuu nchini KTN, NTV, Citizen TV na QTV pamoja na masafa ya dijitali yaliyotolewa kwa runinga hizo. Vyombo hivyo vya habari vilitakiwa  kuheshimu masharti yaliyowekwa wakati wa kutoa leseni za kupeperusha masafa ya dijitali. Kubwa zaidi lilikuwa tarehe za kuhamia mfumo wa dijitali kusalia kuwa zile zilizoratibishwa na mamlaka ya CAK.

Hatua muhimu na ya mwisho ya kuhamia mfumo wa dijitali iliwekwa katika awamu tatu, awamu ya kwanza ilitekelezwa kuanzia tarehe 31 mwezi Disemba mwaka uliopita. Maeneo yaliyohamia mfumo wa dijitali ni Nairobi na viunga vyake….awamu ya pili ilitekelezwa tarehe mbili mwezi huu wa Februari; maeneo yaliyohamia mfumo wa dijitali ni Mombasa,Malindi,Nyeri, Meru, Kisumu, Webuye, Kakamega, Kisii, Nakuru, Eldoret, Nyahururu, Machakos, Narok na Rongai, awamu ya tatu itatekelezwa tarehe 30 mwezi machi na maeneo yatakayolengwa ni Garissa, Kitui, Lodwar, Lokichogio, Kapenguria, Kabarnet, Migori, Voi, Kibwezi na Namanga.

Wakenya wengi wamesalia kwenye giza totoro ambapo  hakuna ajuaye linaloendelea kwenye janibu mbali mbali  za nchi  ila tu kupitia mitandao ya kijamii na runinga mathalan ya K24 na KBC na baadhi ya stesheni nyingine zilizozinduliwa hivi majuzi.

Kila mwamba ngoma huvuta upande wake, wanasiasa pia hawajaachwa nyuma kwenye kizaazaa hiki. Kinara wa Cord bwana Raila Odinga aliisthutumu serikali ya Jubilee kwa kutowajibika vilivyo kuhusiana na suala hili zima. Bwana Raila aliwataka wadau husika wasuluhishe mzozo huo kwa dharura au wakenya wajichukulie hatua wenyewe kwa kuandamana kwa ajili ya suala hilo.

Mwelekezi mkuu wa mamlaka ya  CAK bwana  Francis Wangusi amekiri kuwa hatatatishwa na hatua yoyote itakayochukuliwa na runinga hizo. Bwana wangusi alisema ni runinga hizo zenyewe ambazo zilikiuka sheria.

Wengi wanasubiria ni hadi lini runinga hizi zitadumu kwenye ulimwengu wa giza. Inadaiwa kuwa kupitia  matangazo kampuni hizi zimepoteza mabilioni  za pesa. Hata hivyo zito hufuatwa na jepesi makadirio haya yanasuburiwa na wengi kwa hamu kuu huku kileleta chake kikitarajiwa kung’oa nanga mahamani.

Related posts