October 23, 2018

Maisha Kitendawili

confusion

Imeandikwa na Florence Chanya

Hakuna siku ipitayo bila mimi kuketi kitako na kujisaili kama kuna siku ambayo kila jambo litakuwa limenyooka. Mafumbo ni mengi tu ya kufumbwa na kufumbuliwa. Vitendawili vipo vya kutegwa na kuteguliwa. Vipo ambavyo havina majibu kabisakabisa. Chukua kwa mfano; mioyo ya watu. Insi huyu atakwambia hivi na kumbe anamaanisha vile. Huwezi kukifungua kifua chake uhakikishe moyo wake umeshikilia msimamo upi. Hata wanasaikolojia wenye tajriba si kidogo wanaweza kushindwa kujua kilicho moyoni.Wahenga wa nyakanga za zama walisema kuwa shingo huvaa mkufu. Moyo je? Moyo huvaa nini? Hicho ni kitendawili.

Siwezi kuhesabu nyakati ambazo unawaona watu wakitia bidii za mchwa katika jambo. Wanafanya kila linalotakikana. Kuomba wanaomba, kwa dhati ya mioyo yao. Subira wanayo ambayo hatimaye haivuti heri. Najua watu hao hujisaili, “Ni nini kilichobaki ili mambo yawe barabara?” Ipo hadithi ya watu wawili; mume na mke. Walikwenda kwa mganga siku ya kwanza wakitaka mtoto lakini watu walikuwa wengi wakapewa ahadi ya siku nyingine. Wakaenda siku ya pili. Watu walikuwa wengi zaidi. Waliposongea karibu wakafahamishwa kuwa walikuwa wamefika matangani. Mganga alikuwa ameenda kuzimu bila kafara wala matwana! Tena bila kuwatatulia tatizo lao lililowakosesha usingizi. Hicho kwao kilikuwa kitendawili kikuu.

Gafla kama ajali, kuinamako pia huanza kuinuka wakati hukufanya hili wala lile kufanikisha. La hasha, uliketi kitako na bahati ambayo hukuilalia wala kuiamkia ikabisha hodi. Je, Maulana ndiye aliyemkumbuka mja wake ambaye hata kivuli chake hakijawahi kuvuuka mlango wa kanisa? Ama Ibilisi ndiye anayeaibishwa kwa kumtesa kwa muda mrefu mno mwana wa Mungu? Lakini si Rabuka ndiye muweza na Muumba wa vyote. Kwa nini basi anampa huyu na kumnyima yule. Kwa nini nchi hii iwe na mvua nzuri na mazao na ile nayo ikaushwe na kiangazi? Mambo haya yote ni kitendawili kwangu.

Wapenzi wa Kiswahili hawakuwa kwenye gonezi la pono walipochanja ndimi zao na kusema, “ganda la muwa la jana, chungu kaona kivuno.” Ni mara ngapi kitu ambacho mmoja amekipuuza na kukizika katika kaburi la sahau kinamfaa zaidi mwingine? Ama kitu ambacho mmoja hakihitaji kabisa kinamwauni mwenzake kwa njia ya kipekee? Na nyakati ni chache mno ambazo mambo yanasawazishwa. Kwa nini sumu ya huyu imtibu yule? Daima mambo haya yatakuwa kitendawili.

Related posts