October 23, 2018

Kumbukumbu ya Mau Mau Yazinduliwa

731920-01-02

Imetafsiriwa na; FLORENCE CHANYA

Kumbukumbu ya wakenya walioteswa na kuuliwa na majeshi ya Uingereza; wakati wa Mau Mau; miaka ya moja elfu kenda mia na hamsini ilizinduliwa Jumamosi, jijini Nairobi. Kuezekwa kwa mnara wa ukumbusho ni kati ya makubaliano ya mwaka wa elfu mbili na kumi na tatu, nje ya korti, ambapo Uingereza ilikubali kulipa pauni milioni ishirini za uingereza kama fidia kwa ashiki wa Mau Mau. Vile vile ni njia yao ya kuonyesha kuwa wanavijutia vitendo vyao vya kinyama vilivyosababisha maafa na uchungu wakati mkoloni alipotutawala.

Maelfu ya wakenya wakiwamo watu waliopigania uhuru walifurika furifuri kwenye sehemu hiyo ya ukumbusho, Nairobi ili kushuhudia tukio hilo la historia.

Maelfu ya Wakenya waliwekwa korokoroni wakati hali ya dharura ilipotangazwa ili kupambana na kampeni za Mau Mau. Jambo hili lilisababisha maafa makubwa kwani watu wengi waliyapoteza maisha yao wakipigania uhuru wa nchi hii, ambayo sasa imejisimamia. Wengi waliishia kuchapwa kichapo cha mbwa, kubakwa, kuondolewa mapumbu na hali kadhalika kufanyishwa kazi za sulubu.

Mnara huo wa ukumbusho ni ishara ya upatanisho wa serikali ya Uingereza, Mau Mau na wote walioteseka wakati huo wa hali ya dharura,”alisema Christian Turner, Kamishna mkuu wa Uingereza.

Wazalendo waliomiminika kwenye uwanja wa uhuru, pamoja na familia zao walivalia tishati zenye maandishi, “Shujaa wa Mau Mau” kumaanisha kundi lililopigana dhidi ya utawala wa Waingereza. Katikati ya mnara huo, ipo sanamu ya mpiganaji wa Mau Mau akipokea chakula kutoka kwa mwanamke aliyebeba kikapu cha kitamaduni. Hawatazamani ana kwa ana; ndiposa wasitambuane endapo watashikwa na askari wa Uingereza.

Ashiki kindakindaki na familia zao waliuzunguka mnara huo pindi tu ulipozinduliwa ili kuupiga picha. Nyuso za wengi zilionyesha kuridhika. Kwao tukio hilo la ukumbusho ni ishara ya upatanisho.

Kulingana na Tume ya Kenya ya Haki za Kibinadamu, zaidi ya Wakenya elfu tisini waliuliwa, au wakateswa na mia moja na sitini elfu wakafungiwa mahali pasipofaa kuishi binadamu.

(Tafsiri ya Mau Mau Memorial Unveiled in Nairobi, Derrick Kiplagat)

Related posts