October 23, 2018

Kuhifadhi Kilicho Chako

chivalry

Mwandishi: Florence Chanya

Miongoni mwa walimbwende ilikuwa rahisi mno kumtambua Zuhura. Binti huyo aliumbwa akaumbika; macho ya chawa, shingo la upanga, umbo la mkatiko wa nambari nane na miguu iliyokatwa vizuri na mkono wa maumbile. Alipotabasamu uso ulichanua na sauti yake ya kinanda ingemtoa nyoka pangoni. Ah, jamani Mungu ampe nini amnyime nini?

Zuhura alikuwa changu doa pia! Tena katika miaka ya kisogoni kabla dunia yetu hii haijapiga hatua kiteknolojia kama ilivyo sasa. Basi jioni angejikwatua kwatukwatu. Nguo alizovaa nazo zilimkubali. Zilimchukua kama kitanda kupata mkeka. Angetoka huyo kwa miondoko ya njiwa hadi mtaa wake, akasubiri “kazi.” Haingemchukua muda kuandamana sako kwa bako na kazi yake hiyo; hadi kwenye danguro rasmi. Huko angelipwa kabla ya kumhudumia mteja wake.

Pindi miezi ilipounda miaka ndivyo Zuhura alivyozidi kuwa mrembo-na mjaja kama sungura. Badala ya kutwaa malipo tu, alizindua njia mwafaka ya kujiongezea darahima. “Wanaume wana pesa; nami nina mahitaji,” angejisemea mara kwa mara, “Wasiponidondolea donge nono wenyewe, nitawadondoa mwenyewe,” akaongeza. Angehakikisha wamepiga mtindi nusura uwapeleke wasikorudi, kisha baada ya kazi, walipokuwa katika usingizi wa pono angewapora na kuondoka kimyakimya.

Siku ya siku iliwadia. Alijipatia mwanamume kama kawaida na wakajitoma katika hoteli moja ya kifahari. Baada ya kujivinjari Zuhura alimtaka radhi mwenzake akaenda msalani. Kabla ya bwana huyo kulala alizitoa darahima zake zote na kuzitia mfukoni mwa nguo zake mrembo huyo. Zuhura akarejea na wakalala. Kama kawaida binti huyo aliamka usiku wa manane kuzitafuta pesa kwenye mifuko ya mteja wake. Akaambulia patupu. Ilikuwa sawa na kumtafuta paka mweusi gizani, utampata wapi? “Hawa ni wale mafukara wasio na be wala te,” akang’amua. “Mbona niwe na bahati mbaya hivi?” Akajisaili kwa kukata tamaa, kisha akalala.

Kabla ya ndege kikwara kupasua wingu yule mteja wake alimwamsha na kumtaka watoke akamnunulie kiamsha kinywa kabla ya kila mmoja kushika hamsini zake. Binti akasonya. “mh! Utaninunulia kwa ngwenje gani nawe kando na malipo yangu huna hunani.” Yule bwana akatabasamu na kumwambia asikonde. Haya wakaenda. Wakajipatia staftahi. Ulipowadia wakati wa kulipa yule mteja akamwambia Zuhura achukue fedha kutoka kwenye mfuko wa kushoto wa kirindangoma chake. Kwa kuchanganyikiwa binti akatii na mkono wake ulipotoka humo ulikuwa umeshikilia shilingi elfu kumi, pesa taslimu! Mwanamume huyo alimtupia jicho la dharau Zuhura, akazitwaa zile pesa akampa mhudumu wa hoteli elfu mbili za staftahi na mia tano za huduma. Zingine alizitia mfukoni mwake huku akimnong’onezea Zuhura, “Ukitaka kuhifadhi kilicho chako, kitie mfukoni mwa mwizi; kitakuwa salama.” Kisha alimtakia siku njema na kuondoka bila kuangalia nyuma.

Related posts