October 23, 2018

Jukumu la Baba kwa Mabinti

418540_356151784408914_116624351694993_1260519_1344135260_n

Translated by;
FLORENCE CHANYA MWAITA

Mara si haba kina baba wanaonekana kama mfano bora kwa wavulana wao na wanasemekana kuwa nguzo muhimu katika maendeleo na ukomavu wa maghulamu yao toka utotoni hadi utu uzima. Umuhimu wa wajibu wa kina baba katika maisha ya watato wao wa kiume umesababisha kutotilia mkazo umuhimu wao katika maisha ya watoto wao wa kike. Watoto hujifunza kutokana na mazingira wanayoishi na huchukulia mambo yanayofanyika katika familia kuwa ya kawaida. Katika utangamano wa wasichana na baba zao, ndipo watoto wa kike hao hupata mwelekeo wa matarajio yao kutoka kwa wanaume na mtazamo walio nao kuhusu wanawake.

Msichana atapata picha ya jinsi uhusiano wake na mwanamume utakuwa siku za usoni kwa kuwaona wazazi wake wanavyohusiana. Katika hatua za kwanza za kupanda ngazi za utu uzima kutoka utotoni, wasichana hujifunza kwa kuyatazama kwa kina majukumu ya wake na waume na hasa jinsi ya kuwa katika uhusiano na mwanamume.

Wasomi na waandishi wa vitabu hawajasita kuandika vitabu wakielezea majukumu ya kina baba kwa watoto wao wa kike. Huenda vitabu hivi vimeandikwa katika nyakati na mazingira tofauti ya dunia yetu hii, hata hivyo hapana shaka kuwa hao wote wanakubali kuwa msichana anamhitaji baba katika maisha yake ili akue kiakili na katika nyanja zingine.

Dkt. Marie Hartwell, mwanasaikolojia na mshauri wa familia, anashikilia kuwa kuna kanuni kumi za uwajibikaji wa kina baba.

1. Mpende mamake
Kama Baba unapaswa kumpenda mamake binti yako bila masharti. Mapenzi yako yawe sawa kama si zaidi ya yalivyokuwa mlipokutana kwa mara ya kwanza, hata kama mama mwenyewe haonyeshi upendo huo kwako. Mwanamume anaweza kuishi maisha ya heshima yanayomwonyesha binti yake kuwa siku zote mwanamume yuko tayari kuwa katika mstari wa mbele katika kuwaheshimu wanawake na katika majukumu yake kwa watoto wake.

2. Ziba pengo kati yako na binti yako
Wasichana wanaojiheshimu zaidi ni wale waliokuwa na uhusiano wa karibu zaidi na baba zao walipokuwa wakikua. Kwa hivyo baba yeyote yule anapaswa kuchukua fursa hiyo kwa kutenga wakati wa kuwa na binti yake na kila mara akimkumbusha anavyomjali na kumpenda kwa maneno na vitendo.

3. Kuzipa pengo kuliko salama
Kina baba wataonyesha mfano mzuri na vizingiti visivyofaa kuvukwa; pendo la ukweli au la kuwadhulumu wanao. Mara kwa mara tunasikia wanawake wakilimbikiziwa mzigo wa kuhujumiwa kimapenzi. Ati walisababisha wenyewe! Njia mwafaka ya kuzuia kudhulumiwa ni kumfundisha bintiyo kujua mipaka inayoweza na isiyoweza kuvukwa hasa kwa mtazamo wa kiume.

4. Isherehekee akili yake
Msomee binti yako vitabu anavyopenda na utie juhudi za kufahamu anachosoma shuleni ukipatia nafasi ya kwanza vitu vinavyomsisimua. Kuwa mstari wa mbele katika kuwafahamu marafiki wake, halikadhalika, fahamu uraibu wake. Babamtu anapaswa kusifia chaguo zuri la binti yake huku akimwongoza anapoteleza.

5. Usiyasusie matukio yake
Mwanamke hufurahia mno anaposherehekea nyakati za kipekee na awapendao zaidi. Mabinti haswa wanawahitaji baba zao washuhudie talanta, bidii na ushindi wao. Kina baba, tilieni jambo hili mkazo; mafanikio ya mabinti zenu ni ya kufurahikiwa na kutanuliwa kifua.

6. Mwambie ni mlimbwende
Mila na itikadi zimewasababisha wanawake kutozithamini sura zao. Unapomsifia vizuri binti yako unamjenga kiasi cha kuwa jasiri na kujipenda mwenyewe.

7. Mwonyeshe kuwa mwanamume kamili anaweza kuweka tofauti zake kando na wanawake
Kama mzazi wa kiume, unapokuwa miongoni wa marafiki au wanawake wa aila yako, mwonyeshe binti yako kuwa migogoro inaweza kusuluhishwa kwa njia mwafaka, kwa mfano jinsi wanaume watajihusisha naye. Kwa njia hiyo haitakuwa vigumu kwake kuwashinda wafedhuli akifahamu kuwa wake na waume wanaweza kusuluhisha tofauti zao bila fujo.

8. Unavyotaka afanyiwe bintiyo, wafanyio wanawake wengine
Usiwe domo kaya kuwaponza wanawake mbele ya binti yako. Mtazamo wa baba mzazi kuhusu wanawake, hasa waliokaribu na mabinti wake huziunda akili za wanawe. Mtazamo wa baba mzazi kuhusu wanawake ni pamoja na mtazamo ataoukaunda binti yako kuhusu binafsi yake.

9. Unavyotaka afanyiwe na mumewe, mfanyie wewe
Jinsi baba mtu anavyohusiana na binti yake ndivyo msichana huyo atakavyozoea kuhusiana na mwanamume mwingine. Usimwonyeshe bintiyo kuwa yeye si lolote si chochote. Haifai yeye kuonyeshwa upendo atakapoolewa tu; upendo uliompoka alipokuwa akikua. Kina baba duniani kote wanapaswa kuwachukulia mabinti wao kama malkia.

10. Kuwa mfano mzuri wa mwanamume, unayetaka amwoe bintiyo
Atakapoanza kutafuta mchumba,au kuolewa bintiyo atamtafuta mwenye hulka yako. Kina baba ndio mwongozo wa uume. Mtahadhari sana kwani hapana shaka watawatafuta wachumba wanaofanana nawe kama shilingi kwa ya pili. Kwa hivyo, kwa ajili ya mabinti zenu nyinyi wenyewe muwe wanaume wa kutajika.

(Tafsiri ya Daughters Need Fathers, Too….Iliyoandikwa na Jeanne Ongiyo)

Related posts