October 23, 2018

JE, UNA IMANI NA SERIKALI?

Uhuru signs

Imetafsiriwa na; FLORENCE CHANYA

Serikali ni mfumo unaoiongoza jamii au nchi. Katika mataifa ya Jumuiya ya Madola, neno serikali humaanisha jumla ya kikundi cha watu kinachotekeleza mamlaka ya utendaji katika nchi.

Maelezo haya yanawaweka kando wasanii, vizito, almaarufu kama “socialites” na wacheshi ambao huwasababisha vijana kuvitazama viwambo vya runinga bila kubanduka. Huutazama mfululizo wa filamu na kashfa ndiposa wapate umaarufu au masingizio kwa kipimo sawa. Lakini mambo haya yote huchukua nafasi ndogo ya siri iliyobaki katika bongo zetu mwisho wa siku hiyo. Kwa upande mwingine serikali huzitawala siku zetu nzima kupitia kwa vitengo vyake vitatu.

Sina nia ya kuwahutubia kuhusu elimu ya uraia. Hebu niiseme kwa kifupi kazi ya vitengo hivi. Bunge lililo na wanasiasa waliochaguliwa linahusika na kutayarisha miswada, kuisindika iwe sheria na kuirekebisha ili iwahudumie wananchi. Kwa hivyo wakati mwingine, wanapokwambia kuwa kumiliki silaha bila leseni ni hatia, hawa ndio wanaoifanya gange hiyo.

Kitengo cha utendakazi huwa na rais, naibu wake na baraza la mawaziri na kazi yao ni kushinikiza sheria zilizowekwa na bunge. Katika swala la silaha isiyo halali, waziri wa usalama na mambo ya ndani ndiye anayetoa mwelekeo kwa vyombo husika vikakupoka silaha yako au ukaisajili…au mambo yakabaki vilevile.

Hatimaye mahakama huzisikiliza kesi na kutoa hukumu ipasavyo kwa waliovunja sheria. Hivi ni kama kusema, kuamua endapo mtu atafungwa au la kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Vitengo hivi vitatu vya serikali vinapaswa kukuhudumia wewe, mwananchi wa kawaida na kuboresha maisha. Je, yanafanyika? Kenya imekuwa nchi huru kwa zaidi ya miongo mitano sasa na swali ni, je, tuna imani na serikali?

Historia Mbalimbali

Achilia mbali kuwasili kwa Vasco da Gamma katika pwani ya Kenya, ugunduzi wa mlima Kenya wenye kutilia shaka and porojo zingine. Niwakutilia shaka kwa minajili Bwana Johann Krapf alipowasili kwenye mlima huo mwaka wa moja elfu mia nane na arobaini na tisa aliwakuta watu pahali hapo. Haya tuitembelee historia nyingine.

Mnaikumbuka sakata ya Goldenberg? Ni sawa kabisa kuiita historia kwa kuwa tangu kutukia kwake, watoto walizaliwa na sasa wamekuwa vijana na bado haijasuluhishwa. Mara kwa mara inagonga vichwa vya habari. Hasa kama hakuna jambo jingine la kupigia debe.

Maswali yameulizwa na hati zikawasiliswa kwa vitengo vyote vya serikali lakini tumeambulia patupu. Alalaye amelala usingizi wa pono, akisubiri aamshwe. Kila kukicha tunalalamikia kunyanyaswa bila kufahamu tunachokizungumzia. Tunaapa ya kwamba katu hatutawapigia kura waliohusika. Nyakati zingine tunaandamana na kufunga barabara. Tunaleta msongamano mkubwa. Lakini bure bilashi. Siku mbili baadaye tunazungumzia jinsi kizito mmoja alivyomtenda mtu mmoja mashuhuri.

Historia nyingine ni ya Kashfa ya Anglo-leasing. Mtindo ni mmoja, jina ni tofauti. Kwa mara nyingine tunalalamikia kucheleweshwa kwa kesi, tukisubiri wenye hatia watajwe, waaibishwe na kushtakiwa. Tunashikilia pumzi kwa matarajio kisha…picha za mtu uchi zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii, na tunasahau ibilisi wetu.

Ninaanza kuikubali dhana kuwa, vizito ni wakombozi. Wapo kwa ajili ya kuliauni taifa hili lisije likavurugwa na kashfa za kisiasa. Kwani kunapokuwa na sakata yoyote, wanatuzuzua na vituko vyao. Tunayaacha tuliyo nayo, tunayatazama tuyaonayo! Basi njia hii takatifu ni ya kuonyesha kuwa kila kitu kina madhumuni yake, sivyo?
Hata hivyo, pamoja na vizito na watu mashuhuri wasio na mwelekeo, Kenya inazidi kukumbwa na ufisadi. Mnaukumbuka mgogoro wa kuku?

Serikali ilituudhi mno. Kwa majuma kadhaa tulisubiri tuone vitendo. Hasa kwa kuwa kesi yenyewe ilihamishiwa Uingereza. Wengine walidai haki kwenye mitandao ya kijamii ila waligonga mwamba. Wengine walidhania serikali ilikuwa ikicheza mchezo wa “subiri-uone,”. Wengine wakafikiria itazikwa katika kaburi la sahau. Labda hatutawahi kuujua ukweli.

Tulishusha pumzi Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi ilipofika ugani. Ikasema kama kawaida, “tutafanya uchunguzi”. Kisha wakatakiwa, kwa heshima, kung’atuka nyadhifani. Je, ni mchezo mchafu? Tutasubiri kama kawaida, tuone. Ila tunajua mambo ya kuku yanahusu nini, sivyo?

Walipatikana

Vyombo vya habari vimekuwa macho ya wananchi na nyakati nyingi hufanya kazi ya kutajika. Wakati mwingine vinanyongwa lakini hutoka katika kitanzi na kuwaambia wanaowaombea mauti, “kajaribuni tena”.

Vyombo hivi huru hutuondolea imani kwa serikali yetu. Akili yangu inalizuru duka kubwa la Westgate na jinsi lilivyozingirwa Septemba, tarehe ishirini na moja miaka miwili iliyopita. Vilijaribu kutuletea habari za matukio hayo katika hali ngumu mno. Serikali ikitengeneza hapa na pale, kadri ya uwezo wake lakini Wakenya waliona tu serikali iliyochanganyikiwa. Toka kwa masimulizi ya kuchekesha hadi kwenye upayukaji wa mawakala wa serikali waliotoa ripoti; kuzuiliwa kwa wanahabari katika sehemu hiyo, sarakasi za polisi na jeshi na halikadhalika ushujaa wa mwananchi wa kawaida. Kilikuwa kizungumkuti.

Tulipigwa mafamba, tukapakwa mafuta kwa mgongo wa chupa na tukahadaika. Tukaamini kuwa magaidi walizuiliwa ndani ya jengo hilo kwa siku nne na wakafa siku ya nne. Halafu wanahabari wakafanya upelelezi wao na imani tuliokuwa nayo kwa serikali ikaanza kuyeyuka. Magaidi walinaswa na kamera za CCTV siku ya kwanza peke yake. Kwa hivyo siku tatu zilizofuta, tulikuwa tumemzuilia nani? Wanajihadi hawanywi tembo, ni nani alipiga mtindi kwenye duka hilo? Mnaikumbuka mifuko ya karatasi?

Hatua za usalama zilichukuliwa ili kupambana na ugaidi baada ya hayo. Hatua hizo zilifaa sana hivi kwamba shambulizi kama la kigaidi lilipotokea huko mpeketoni mwaka uliopita, serikali ilishikilia kuwa lilichochewa kisiasa. Bila shaka rais akaahidi kuwasaka wahalifu, haki itendeke. Wengi wakamwamini na wachache wakawa na tashiwishi.

Hivi karibuni imeundwa video ambayo imeichanachana bidii ya rais katika suala hilo. Ni kazi ya wanamgambo wa Al-Shabaab ambao wanaelezea kinagaubaga shambulio hilo, mauaji ya kinyama na onyo kali kwa Wakenya: wasidhubutu kuingia Somalia. Imeundwa na mtaalamu na imehaririwa na mtu stadi kumaanisha kuwa kundi hilo la kigaidi lina rasilimali, na sio za kivita peke yake.

Kwenye video hiyo, wanamgambo hao wamewaita waongo na wezi wanasiasa wa Kenya. Wanakiri kuwa ndio waliopanga shambulizi na mengine yatafuta. Kwa hivyo swali tunalopaswa kujisaili ni; je, tutamsikiliza rais baada ya janga kutufika? Je, serikali hutudanganya makusudi ili kutuepusha na janga ama ni mazoea tu?

Hivi sasa

Kuna mambo kadha wa kadha leo hii, katika uwanja wa umma na ambayo yameimulika serikali. Kuna tuhuma zinazoielekea Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi na kamati ya Akaunti ya Umma. Kuna mgogoro usioisha wa kampuni ya sukari ya Mumias na kashfa ya Anglo-leasing pia. Usitutoke uchunguzi wa mauaji ya mwanasiasa, George Muchai. Inadaiwa alipigwa risasi na barobaro mwenye macho mekundu na mtindo wa nywele wa rasta! Yapo mauaji ya George Saitoti, Orwa Ojode, JM Kariuki na wengine wengi.

Kama kawaida wanasiasa wa pande zote za serikali huahidi kutangaza hadharani ukweli kuhusiana na vifo hivyo la sivyo wajiuzulu endapo haki haitatendeka. Je wao hufanya hivyo? Jicho la umma sasa limemmulika mwenyekiti wa Kamati ya Akaunti ya Umma, Bwana Ababu Namwamba na rekodi yake ya siri. Ni muda gani hadi kizito atuzuzue, tupumbazike,tuangalie kwingine? Na pamoja na hayo, una imani na serikali?

Related posts