October 23, 2018

IWAPI NAFASI YA MTOTO WA KIUME?

timthumb.php

Imetafsiriwa na; FLORENCE CHANYA
Je ni kosa la msichana? Ama ni uchu wa mwanamume usiokadirika?
Je, ni chaguo la nguo la binti? Ama ni mwanamume hajatoshelezwa?
Je, ni benati anatongoza? Ama mwanamume anautanulia kifua uume wake?
Je, ni makubaliano? Ama ni swala la mtu kutaka kibali?
Ni maafikiano ya kibiashara? Ama watu wanajivinjari?
Ni malipo ya kitu?
Ni kutega uchumi?
Ni ngono tu?

Matukio yanayotangulia ubakaji hayawezi kuelezeka. Mbakaji na mdhulumiwa ndio wanaoweza kutueleza kinagaubaga matukio hayo. Ndio peke yao wanaoweza kushuhudia. Watuhumiwa wanaweza kujieleza na pia wanaweza kutoa kadhongo wafichiwe uovu huo. Wakajitanibu kabisa na kitendo hicho cha unyama. Huwaacha walalamishi katika vita vya, “Alisema kuwa binti huyu alisema vile” maadamu mbakaji na mlalamishi ndio mashahidi pekee wa uovu huo.

Mabenati huwa na ndoto nyingi maishani. Kila uchao wanatumainia kuwa watu wa kutajika; na kubakwa hakupo kabisa katika mipango yao ya fanaka. Kwa hivyo wanapotendewa unyama huu, nafsi zao huwa zimevyogwa na kufyandwafyandwa; na huachwa na kovu la aushi.

Huenda hatutawahi kuelewa jinsi wanawake au wanaume hufikiria. Kinachompa huyu motisha hakimpi yule. Kwa hivyo jambo la kwanza tunalojisaili ubakaji unapofanyika ni, “Aalivalia vipi binti huyo?” Je, ubakaji hufanyika kwa ajili ya mavazi aliyovalia mwanamke? Mara kwa mara wanaume husemekana kuwa huvutiwa sana kwa kuona tu, kinyume kabisa na wanawake. Lakini mavazi hayapaswi kuwa kigezo cha kuamua kesi ya ubakaji. Wanaume wanaweza kuvutiwa na sehemu tofauti. Kwa wengine, kuiona sehemu fulani tu ya mwili kunatosha. Wengine huvutiwa na kifua, wengine kiuno na wengine nywele pekee. Kwa msingi wa mtu kuwa mwanamke tu, wanaume wengine hupagawa. Kwa hivyo, tunapotoa hukumu zetu zisizo na mashiko, kuhusu ubakaji, tusiwe tunawalimbikizia lawama mabinti kwa namna walivyovaa.

Wanaume wamelaumiwa mara si kidogo kwa ubakaji lakini hebu tuutazame upande wa pili. Tutasemaje kuhusu wanaume wanaonajisiwa? Je tumewahi kuwafikiria? Mwanamume anaweza kudinda kuliweka hadharani jambo kama hilo lakini naamimi kuwa wao pia hufanyiwa unyama huu.Je, jamii huwachukulia vipi wanaume kama hao? Wanyonge walionyong’onyea! Kwa lugha ya mitaani wataulizwa, “unawezaje kumwacha mwanamke akukalie?” Tangu jadi wanaume walijulikana kama watu ambao huficha matatizo yao. Badala ya kusema wakautua mzigo, huungulika ndani kwa ndani na huenda siku moja wakalipuka. Hivi kwamba hawaambiliki wala kusemezeka. Hawasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini.

Mtoto wa kike alipodhulumiwa, ndani hakukukalika; na nje vile vile kwani mashirika ya kuwatetea wanawake yalizinduliwa. Kwa sababu hiyo, mtoto wa kiume ametelekezwa. Nani atasimama kidete kumshughulikia? Ni nani atampatia uwezo wa kujisimamia? Je, tunaweza kuwa na mashirika ya maendeleo ya watoto wa kike na wa kiume? Inawezekana. Mashindano halisi ni ya makundi mawili au zaidi. Lakini mashirika ya kuwaendeleza wanawake yapo ugani yakicheza dhidi yao wenyewe. Je, inawezekana wanaume wakaingia uwanjani wachezee upande wa pili kwa kuyazindua mashirika yao? Kwa nini tusiwe na hospitali za wanaume kana tulivyo na za wanawake?

Hebu tuwafikirie wanaume pia na tukome kumpendelea mtoto wa kike huku wa kiume akitupwa katika kaburi la sahau. Tunaitia jamii yetu doa bila kujua. Hebu tumkumbuke mwanamume aliyesahauliwa katika harakati za kuwaendeleza wanawake. Na ambaye hana mbele wala nyuma kwasababu aliwekwa pembeni na jamii nzima siku za kisogoni. Tusiwaache wanaume wetu wafe kikondoo kwa kuwa jamii ilikoma kuwajali kama mtu anavyokoma kunyonya.

(Tafsiri ya ‘Who’s Fault is Rape?’… Vera Marion)

Related posts