July 09, 2020

CHAGUO NI LA MTU BINAFSI; ILA MILA NA ITIKADI ZA JAMII ZINAPOATHIRIWA

Supreme court gay marriage

Imetafsiriwa na FLORENCE CHANYA

Kuwa mahakama kuu ya Kenya; iliilazimu bodi inayosimamia shirika lisilo la kiserikali kukisajili kikundi cha watetezi wa haki za kibinadamu; kinachowawakilisha wakenya mashoga na wasagaji tarehe ishirini na nne, Aprili, mwaka huu, sio habari sasa. Wakitetea uamuzi huo, majaji hao watatu walishikilia kuwa bodi ya shirika hilo, ilifanya kinyume na katiba ya Kenya kwa kukosa kuwafanyia haki na usawa mashoga na wasagaji wanaoishi Kenya na wanaotaka muungano wao usajiliwe. Waliongeza kuwa sheria haiyumbi katika kulinda haki za walio wachache nchini.

Tukiachilia mbali maswala ya Idara ya mahakama na katiba, hebu, tuliangalie swala hili kwa kifupi. Kwa kutumia wingi ningependa mfahamu ya kwamba ninawazungumzia Wakenya wenye maoni kama niliyo nayo na sio kuyatia katika kapu moja la maoni ya watu wote.Kenya, kama nchi zingine za Kiafrika husita kuyazungumzia maswala ya ngono. Ni mwiko kuyazungumzia mambo haya, hasa hadharani. Ukweli huo unaweza kufahamika mja akizitazama nyuso za Wakenya wanapokumbana uso kwa uso na vipindi kama hivyo kwenye runinga, hasa watu wa aila moja.

Kama ni mwiko kulizungumzia swala la ngono hadharani, sielewi tulikopata ujasiri wa kuwazungumzia mashoga na wasagaji jambo ambalo limepokelewa kwa hisia tofauti na Wakenya.

Nina hakika kuwa kabla ya mjadala huo wa kundi hilo la wachache; kama wanavyoliita wanasheria, kuufikia umati liliendeleza vitendo vyao na mambo yalikuwa barabara. Achilia mbali vizingiti vya hapa na pale vinavyoshuhudiwa na binadamu yeyote yule. Yamekuwepo maandamano kadhaa ya kundi hilo, likilalamikia kunyanyaswa na ukosefu wa usawa. Kwa maoni yangu badala ya swala hili kuletwa hadharani lingeshughulikiwa pembeni na baada ya majidiliano wanaozitetea haki zao wakawasajili katika utimilifu wa nyakati. Kenya ni nchi ya mchanganyiko. Ina dini tofautitofauti na bila shaka hakuna dini inayoruhusu ndoa za namna hiyo.

Vyombo vya habari huweka ajenda na pia ni kioo cha jamii na pasipo jingine vinaweza kuonekana kana kwamba vinaieneza kasumba kuwa Wakenya wote wameukumbatia ushirikiano wa kimapenzi wa jinsia moja, kumbe la hasha. Kibaya zaidi ni mvutano kati ya serikali na Idara ya mahakama iliyopewa mamlaka na serikali: inawaunga mkono, huku serikali kuu ikiongozwa na naibu wa rais, William Ruto, ikijitanibu na kundi hilo la wachache. Kama Wakenya tunakumbana na kizungumkuti. Je, ushoga na usagaji ni sawa au la? Tuna mfano gani kwa vijana na vizazi vijavyo? Tunakiambia nini kizazi cha jana ambacho hakijawahi kung’ang’ana kuyajadili mambo kama hayo? Je, ni mtindo wa maisha tunaofaa kuuzungumzia kadamnasi?

Binafsi yangu ninafikiria kuwa, kuwa shoga au msagaji ni chaguo la mtu anavyopenda kujamiiana, na hivyo sio kosa. Lakini ikiwa vitendo vya mtu havilandani na picha ya nchi au vitaisababishia nchi nzima kupata sifa mbaya, ni vyema swala hilo lishughulikiwe katika chemba. Hatimaye, natumai kuwa kikundi hicho cha kutetea haki kitasajiliwa na hali kadhalika kitafanya haki na kukomesha unyanyasaji wa mashoga na wasagaji. Lakini, kisivuke mipaka kwa kuanza kukipigania kibali cha kutambuliwa kwa ndoa za jinsia moja. Kenya ni nchi ya bara la Afrika inayojisimamia, na kuyatilia mkazo yaliyo mema. Ikiwa tunaona soni ya kuzungumzia swala la ngono katika panda shuka za maisha yetu kila siku, basi kundi hilo la walio wachache linapaswa kutambua kuwa bado hatujalikubali jambo hilo. Hayo ni maoni yangu tu.

Kama una maoni pinzani, ufanyishe zoezi uhuru wako wa kujieleza, sauti yako na isikike; kwa sababu uhuru wa kujieleza bado unathaminiwa na kulindwa na sheria.

Tafsiri ya: Sexuality Is a Choice, not Unless it Erodes Moral Values In the Society
Kama ilivyoandikwa na: Jeanne Ongiyo

Related posts